February 27, 2026

WatuCrash

📚 Education & Learning Hub (Primary + Secondary)

science

NUKUU ZA SOMO LA SAYANSI NA TEKNOLOJIA DARASA LA TANO

Sifa za Viumbe Hai

1. Kula: viumbe hai huhitaji chakula chenye virutubisho mbalimbali kama vile protini, wanga, mafuta, madini, vitamini na chumvi. Vyakula huvifanya viumbe hai kukua na kupata nguvu. Pia chakula husaidia mwili kujikinga na magonjwa mbalimbali.

2. Kupumua: kupumua ni kitendo cha kuvuta hewa safi ndani na kuitoa hewa chafu nje ya mwili wa kiumbe hai. Wanyama huvuta hewa ya oksijeni ndani ya mwili na kutoa hewa ya kabonidayoksaidi nje ya mwili. Mimea pia huvuta hewa ya kabonidayoksaidi na kutoa hewa ya oksijeni wakati wa usanishaji chakula.

3. Kuitikia vichocheo: wanyama huitikia vichocheo kwa kutumia milango ya fahamu ambayo ni pua, ngozi, macho, ulimi na masikio. Mimea huitikia vichocheo kupitia mizizi, shina, matawi, majani na maua. Baadhi ya vichocheo ni mwanga, joto, baridi, mgandamizo, virutubisho vya chakula na maji.

4. Kujongea: kujongea ni kitendo cha kusogea kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine au kubadili uelekeo. Mimea na wanyama hujongea kwa njia mbalimbali. Kujongea kunawasaidia viumbe hai kutafuta makazi yao; kutafuta chakula, maji; kuepuka maadui wao; kutafuta mahitaji ya kujamiiana; uchavushaji.

5. Kuzaliana: kuzaliana ni kitendo cha kuongezeka kwa idadi ya viumbe hai. Wanyama huzaliana kwa njia ya kutaga mayai na kuzaa watoto hai. Mimea huzaliana kwa kutumia mbegu au kuotesha mashina ya vipandikizi.

6. Kutoa taka mwili: viumbe hai hutoa takamwili zilizo katika hali ya hewa na majimaji. Wanyama hutoa maji na chumvichumvi nje ya mwili kwa njia ya mkojo na jasho. Pia hutoa gesi kwa njia ya kupumua.mimea hutoa taka katika hali ya maji, gesi na utomvu.

7. Kukua: kukua ni kitendo cha kuongezeka kwa kimo, uzito, ukubwa na umbo la seli.

Sifa Zinazotofautisha Wanyama na Mimea

1. Kujongea: wanyama hujongea kwa kuhama mwili mzima kutoka sehemu moja hadi nyingine. Mimea hujongea katika baadhi ya sehemu za mmea. Kwa mfano, shina la mmea hujongea kwa kufuata mwanga (fototropizimu), mizizi ya mimea hujongea kwa kufuata maji (haidrotropizimu), mizizi pia huweza kukua kwa kufuata kani ya mvutano ya dunia (jiotropizimu).

2. Kula: mimea hupata chakula kwa kujitengenezea kwa kutumia nishati ya mwanga wa jua, maji na hewa ya kabonidayoksaidi (fotosinthesisi) lakini wanyama hawana uwezo wa kujitengenezea chakula chao wao wenyewe isipokuwa wanategemea chakula kutoka kwa mimea.

3. Upumuaji: wanyama huvuta hewa ya oksijeni ndani ya mwili na kutoa hewa ya kabonidayoksaidi nje ya mwili. Mimea hutumia hewa ya kabonidayoksaidi kwa ajili ya usanishaji chakula na kutoa hewa ya oksijeni.

MAKUNDI YA VIUMBE HAI

Kuna aina mbili za viumbe hai ambazo ni:1. Wanyama

2. Mimea

MAKUNDI YA MIMEA

Miti imegwanyika katika makundi makuu manne. Kati ya hayo, yafuatayo ni makundi mawili:1. Mimea itoayo maua.

2. Mimea isiyotoa maua.

Mimea Inayotoa Maua

Ni mimea ambayo ua ndiyo sehemu maalumu ya uzazi. Ua hubadilika kuwa tunda na tunda kuwa mbegu ambayo hukua na kukomaa. Mifano ni miharagwe, ngano, miembe, njegere na alizeti. Mimea hii hutumika kwa chakula, dawa, kutengenezea nguo na kuni. Pia hutumika kama makazi ya wanyama.

Sifa za Jumla za Mimea Inayotoa Maua

1. Mimea hii ina vifereji vipitishi vya maji na chakula yaani zailemu na floemu vilivyokamilika.

2. Sehemu kuu ya uzazi ya mimea hii ni maua.

3. Mimea mingi hupatikana nchi kavu na mingine kwenye maji.

4. Urutubishaji wa mbegu za uzazi hufanyika baada ya kutengenezwa kwa mrija wa chavua (nelichavua).

5. Mbegu hulindwa na kufunikwa na ovari/tunda.

6. Pia mimea hii huweza kuzaliana kwa njia ya ubebeshaji wa mimea kwenye mimea mingine.

7. Ina mifumo kamili ya mizizi, majani na mashina.

Makundi ya Mimea Inayotoa Maua

Mimea hii imegawanyika katika makundi mawili ambayo yametokana na idadi ya ghalambegu katika kila mbegu.

Makundi hayo ni:-

1. Monokotiledoni: hii ni mimea inayozalisha mbegu zenye ghalambegu/kotiledoni moja.

2. Daikotiledoni: hii ni mimea inayozalisha mbegu zenye ghalambegu/kotiledoni mbili.

Mimea Aina ya Monokotiledoni

Hii ni mimea yenye mbegu ambazo zina kotiledoni au ghalambegu moja. Mifano yake ni mtama, mahindi, ulezi, nazi na ngano.

Mimea hii ina majani yenye vena zilizosambamba kufuata urefu wa jani.

Mizizi yake ni nyuzinyuzi inayoota kwa pamoja kwenye kitako cha shina. Mimea hii hauna mzizi mkuu.

Mimea Aina ya Daikotiledoni

Hii ni mimea yenye mbegu ambazo zina kotiledoni au ghalambegu mbili. Mifano yake ni miembe, maharagwe na kunde. Mimea hii ina majani yenye vena zilizotanda kama wavu. Pia mimea hii ina mzizi mkuu pamoja na mimea mingine midogodogo.

Tofauti kati ya Monokotiledoni na Daikotiledoni

TofautiMonokotiledoniDaikotiledoni
Zailemu na floemuZailemu na floemu ni ndogo na zimesambaa kwenye shinaZailemu na floemu zimepangiliwa katika duara kuzunguka shina
Umbo la majaniIna majani marefu na membambaIna majani mapana
VenaMajani yake yana vena sambambaMajani yake yana vena zilizofungamana na zinazopishana kama wavu
MiziziIn mizizi kama brashi na isiyo na mzizi mkuuIna mzizi mkuu
Idadi ya ghalaGhala mbegu moja ya chakulaGhala mbegu mbili za chakula
Umbo la shinaHakuna kiini kwenye shinaKuna kiini kwenye shina la mmea
Sehemu za uaSehemu za ua zimegawanyika katika makundi matatu matatuSehemu za ua zimegawanyika katika makundi manne manne au matano matano
Ukuaji wa piliIkikatwa haiwezi kuchipua au kuota tenaIkikatwa inaweza kuchipua ama kuota tena
Umbo la uaHaina petali na sepaliIna petali na sepali
MifanoMfano ni mahindi na nyasiMfano ni maharagwe, njegere na soya

Mimea Isiyotoa Maua

Mimea isiyotoa maua ni ile mimea ambayo, maua sio sehemu kuu ya uzazi. Mimea hii haitoi matunda lakini inatoa mbegu.

Mbegu za mimea hii hazifunikwi ndani ya tunda kwa mfano mbani, mvinje na mwerezi.

Mimea hii huwa ya kijani karibu muda wote wa mwaka.

Mimea hii hutumika kwa shughuli za mbao na kuni, kutengenezea karatasi na gundi pamoja na makazi ya wanyama pori.

Sehemu za Mmea na Kazi Zake

Mmea una sehemu kuu tatu ambazo ni mizizi, shina na majani. Sehemu nyingine ni maua, matunda na mbegu.

Mizizi

Kazi:​(i) Kufyonza/kusharabu maji, madini na virutubisho kutoka kwenye udongo.

(ii) Kushikilia mmea kwenye udongo ili usianguke.

(iii) Kuhifadhi chakula cha mmea kama vile kwenye muhogo na viazi vitamu. (iv) Kushikilia udongo na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Shina

Kazi:​(i) Kushikilia majani, maua na matunda.

(ii) Kusafirisha maji, virutubisho na madini kutoka kwenye mizizi kwenda kwenye matawi na majani. (iii) Kuhifadhi chakula cha mmea kama vile miwa.

Majani

Kazi:​(i) Kusanisi au kutengeneza chakula cha mmea na kusaidia kuendelea kukua.

(ii) Stomata zilizoko kwenye majani husaidia kurekebisha kiwango cha maji, oksijeni na kabonidayoksaidi. (iii) Kuhifadhi akiba ya chakula mfano vitunguu na mboga mboga za majani.

Maua na Matunda

Kazi:​(i) Uzazi. Harufu na rangi nzuri ya maua husaidia kuwavutia wadudu kubeba chavua kutoka ua moja kwenda ua jingine. Kitendo hiki huitwa uchavushaji.

(ii) Tunda husaidia kushikia na kufunika mbegu ambayo baadaye hupandwa, huota na kuwa mmea.

MAKUNDI YA WANYAMA

Wanyama wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni:-

1. Wanyama wenye uti wa mgongo kama vile binadamu, ndege, mijusi, samaki na chura.

2. Wanyama wasio na uti wa mgongo kama vile panzi, konokono na minyoo.

Wanyama Wasio na Uti wa Mgongo

Hawa ni wanyama ambao hawana uti wa mgongo kama vile panzi, konokono, kipepeo, minyoo, mende, jongoo, tegu na pweza.

Wanyama hawa hupatikana nchi kavu na majini.

Wanyama hawa wamegawanyika katika makundi yafuatayo:1. Athropoda

2. Minyoo

3. Konokono na ngisi

Athropoda

Ni kundi la wanyama wenye miili iliyogawanyika katika pingili zilizounganishwa.

Wana miguu yenye pingili ambayo hufanya kazi za mbadilishano wa gesi, ukusanyaji wa chakula, kujongea, na kuelekea vichochezi.

Athropoda wana miili iliyogawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni kichwa, kifua na fumbatio.

Mifano ya wanyama wa kundi hili ni kama vile nyuki, mchwa, kipepeo, panzi, nzi, kaa, buibui, tandu na jongoo.

Athropoda wamegawanyika katika makundi mengine madogomadogo kama ifuatavyo:-

• Wadudu/insekta: hupatikana maeneo ya maji maji na wengine nchi kavu; miili yao imegawanyika katika sehemu kuu tatu kichwa, fumbatio na tumbo; wana jozi tatu za miguu na jozi moja ya mabawa; wana jozi moja ya antenna kichwani; hupumua kwa kutumia trakea na matamvua; mifano ya insekta ni kipepeo, mende, nzi, mbu, mchwa na panzi; hupitia metamofosisi kamili yaani yai, lava, pua na mdudu kamili.

• Araknida: hupatikana nchi kavu na baadhi kwenye maji; mwili umegawanyika katika sehemu mbili yaani kichwa/kifua na fumbatio; wana jozi nne za miguu; hupumua kwa matamvua, trakea ama mifuko vya mapafu. Mfano ni chawa, buibui na nge.

• Miriapoda: hupatikana zaidi nchi kavu; wana jozi nyingi za miguu; miili yao imegawanyika katika pingili ndogo ndogo kila moja ikiwa na jozi mbili za miguu; kichwa kina antenna, jozi moja ya macho na jozi mbili au tatu za taya; hupumua kwa trakea. Mifano ni jongoo na tandu.

• Klastasea/kaa: hupatikana zaidi maeneo ya maji maji, nchi kavu na baadhi yao huishi kwenye miili ya wanyama; kichwa kimeungana na kifua hivyo miili yao imegawanyika katika sehemu mbili; hupumua kwa kutumia matamvua. Mfano ni kaa.

Minyoo

Huzaliana kwa kujamiiana.

Hula nyama na baadhi ya vijidudu vidogo vidogo.

Huishi kwenye makazi mbali mbali kama vile kwenye maji, kwenye miili ya wanyama, na kwenye udongo.

Wana mfumo nyoofu wa fahamu.

Miili yao huweza kugawanyika katika sehemu mbili zilizo sawa.

Baadhi yao wana mfumo wa mmeng’enyo wa chakula usio kamili (wana mdomo na hawana puru) na wengine wana mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kamili.

Konokono na Ngisi

Kundi hili linajumuisha wanyama waishio nchi kavu na kwenye maji. Wengine ni pweza na ngisi ambao huishi baharini.

Wanyama Wenye Uti wa Mgongo

Uti wa mgongo ni muunganiko wa pingili za mifupa inayoanzia kisogoni hadi sehemu ya chini ya kiuno au mkiani.

Ndani ya pingili za mifupa ya uti wa mgongo kuna kiini au ugwemgongo ambao ni mwendelezo wa ubongo. Ugwemgongo ni ute wenye neva za fahamu ulio ndani ya pingili za uti wa mgongo. Ubongo na ugwe mgongo huunda mfumo wa fahamu na kufikisha taarifa mbalimbali za mwili kupitia neva.

Wanyama hawa wamegawanyika kwenye makundi matano ambayo ni:1. Samaki

2. Amfibia

3. Reptilia

4. Ndege

5. Mamalia

Samaki

Kuna aina mbili za samaki waishio ndani ya maji.

1. Samaki wanaoishi kwenye majichumvi.

2. Samaki wanaoishi kwenye maji yasiyo na chumvi.

Samaki Wanaoishi Kwenye Maji ya Chumvi

1. Miili yao imefunikwa na mifupa laini pamoja na magamba magumu na makubwa.

2. Pezi la mkiani limegawanyika katika sehemu mbili zinazotofautiana kwa ukubwa.

3. Wana mdomo na jozi ya matundu ya pua yaliyopo kila upande ubavuni mwa kichwa.

4. Samaki hawa huzaliana kwa kutaga mayai.

5. Wana matamvua ambayo hayajafunikwa na gamba gumu liitwalo opekyulamu.

6. Mfano wa samaki hawa ni papa.

Samaki Wanaoishi Kwenye Maji Yasiyo na Chumvi

1. Hawa ni samaki ambao miili yao imefunikwa na mifupa migumu na magamba laini.

2. Wana midomo iliyochongoka na matundu ya pua yapo sehemu ya juu ya kichwa.

3. Wana matamvua ambayo yamefunikwa na gamba gumu liitwalo opekyulamu.

4. Mifano ya samaki hawa ni sangara, sato.

Aina Nyingine za Samaki

• Samaki wenye magamba kama vile perege na ambayo hawana magamba kama vile kibua.

• Samaki wenye mifupa migumu kama vile perege na samaki wenye mifupa laini kama vile papa.

Sifa za Wanyama Katika Kundi la Samaki

1. Samaki wana damu baridi (poikilothemia). Joto lao hubadilika kulingana na mazingira.

2. Baadhi ya miili ya samaki imefunikwa kwa magamba yaliyopandana kuelekea mkiani.

3. Samaki wana mstari wa neva unaowasaidia kuhisi miguso na mielekeo ya mawimbi ya maji.

4. Samaki wana mapezi wanayoyatumia kuogelea na kubadili mwelekeo na mwendo. Mapezi ni viungo vidogovidogo mgongoni, mashavuni na ubavuni mwa samaki ambavyo humwezesha kuoegelea.

5. Samaki hutumia matamvua yaliyofunikwa kwa gamba gumu liitwalo opekyulamu kupata oksijeni iliyo kwenye maji. Matamvua ni viungo vyenye nyuzi nyuzi vilivyo ndani ya shavu la samaki vyenye kazi ya kvuta na kuchuja hewa inayoingia na kutoka ndani ya mwili wake.

6. Umbile la samaki limechongoka kwa upande wa mbele ili kumsaidia kujongea kwa urahisi ndani ya maji.

7. Samaki huzaliana kwa kutaga mayai.

8. Samaki wana utelezi kwa juu unaowasaidia kupunguza ukinzani anapojongea.

Amfibia

• Wanyama waishio majini katika hatua za awali za ukuaji na baadaye nchi kavu. Mfano ni chura.

• Wapo chura anaoishi nchi kavu na kwenye maji.

• Chura hutaga mayai ndani ya maji yasiyo na chumvi.

• Mayai yakianguliwa hutoa lava ambao huishi kwenye maji na kupumua kwa kutumia matamvua. â€¢ Baadaye lava hawa huhamia nchi kavu wanapokuwa wameota mapafu.

Sifa za Wanyama Katika Kundi la Amfibia

1. Amfibia wana ngozi laini yenye unyevu kwa ajili ya kupumulia.

2. Wana viwambo vya masikio pande zote za kichwa kwa ajili ya kusikia

3. Wana matamvua katika hatua za awali za ukuaji (lava) kwa ajili ya kupumua. Wakikua hutumia mapafu na ngozi.

4. Wana damu baridi (poikilothemia) ambayo hubadilika kulingana na halijoto ya mazingira. Hali hii huitwa poikilothemia.

5. Wana miguu minne, ya mbele mifupi na miguu ya nyuma ni mirefu.

6. Wana miguu yenye vidole vinne vilivyounganishwa na ngozi nyembamba.

7. Hutaga mayai ndani ya maji isipokuwa chura wa Kihansi ambao huzaa.

8. Wana midomo mipana kwa ajili ya kuingiza chakula kwa haraka na urahisi zaidi.

9. Wana moyo ambao umegawanyika katika vyumba vitatu.

Reptilia

Reptilia ni kundi la wanyama wanaoishi nchi kavu na majini. Kijusi, nyoka, kobe, na kinyonga huishi nchi kavu wakati mamba, kenge, kasa na baadhi ya nyoka huishi kwenye maji.

Baadhi ya reptilia hujongea kwa kutumia miguu na wengine hujongea kwa kutambaa kama vile nyoka.

Sifa za Wanyama Katika Kundi la Reptilia

1. Ngozi ya reptilia ni kavu na imefunikwa na magamba.

2. Reptilia wana miili iliyochongoka kuanzia kichwani hadi mkiani.

3. Reptilia wana mikia mirefu na miembamba.

4. Baadhi ya reptilia hawana miguu na hujongea kwa kutambaa kwa msaada wa misuli ya tumbo.

5. Reptilia wana miguu yenye vidole vinne au vitano na kucha ambavyo huwasaidia kujongea.

6. Reptilia wana midomo mipana na iliyochongoka.

7. Reptilia hutaga mayai.

8. Baadhi ya reptilia hujibadili rangi ili kujilinda dhidi ya maadui na kuweza kuwinda chakula chake kwa urahisi.

9. Reptilia wana damu baridi ambayo hubadilika kulingana na halijoto ya mazingira (poikilothemia).

10. Reptilia hutumia mapafu kwa ajili ya kupumua.

Ndege

Ndege ni wanyama wenye uti wa mgongo na manyoya. Baadhi ya ndege hufugwa kama vile kuku, bata, njiwa, kanga na kasuku na wengine huishi porini kama vile mwewe, pengwini, kiwi, bundi, kunguru na mbuni. Ndege wengi huishi nchi kavu na baadhi huishi majini.

Sifa za Wanyama Katika Kundi la Ndege

1. Ndege wana miili iliyochongoka nyuma na mbele. Hii humsaidia kuruka hewani bila kupata ukinzani mkubwa na hewa.

2. Mwili wa ndege umefunikwa na manyoya ili kumsaidia kuhifadhi joto la mwili na kuzuia maji yasifikie ngozi.

3. Ndege wana mabawa yenye manyoya marefu yanayomuwezesha kuruka hewani.

4. Ndege wana midomo migumu, mirefu na iliyochongoka (yenye ncha kali).

5. Ndege wana miguu miwili yenye magamba na vidole vinne vyenye kucha ngumu.

6. Ndege wana damu joto isiyobadilika kulingana na halijoto ya mazingira. Hii huitwa homeothemia. Jotoridi la mwili wa ndege ni nyuzi 40za sentigredi.

7. Ndege huzaliana kwa kutaga mayai.

8. Ndege wendi hujongea kwa kuruka.

Mamalia

Mamalia ni kundi la wanyama wenye uti wa mgongo ambao huzaliwa wakiwa viumbe kamili.

Mamalia wana miili yenye vinyweleo. Mamalia wengi huishi nchi kavu. Mamalia wana miguu miwili au minne kwa ajili ya kujongea. Baadhi ya mamalia hujongea kwa kuruka kama vile popo na wengine huishi kwenye maji kama vile nyangumi. Mifano ya mamalia ni binadamu, popo, tembo, mbwa, simba, pundamilia, chui, kangaruu, ng’ombe, mbuzi, nyani na kondoo.

Sifa za Wanyama Katika Kundi la Mamalia

1. Mamalia hunyonyesha watoto wao maziwa.

2. Mamalia wana masikio yaliyojitokeza.

3. Mamalia wana miili yenye vinyweleo kwa ajili ya kutunza joto.

4. Mamalia wana ngozi yenye tezi za jasho isipokuwa nyangumi.

5. Mamalia wengi huzaa watoto walio hai. Baadhi ya mamalia hutaga.

6. Mamalia hutembea kwa miguu minne isipokuwa binadamu.

7. Mamalia wengi huishi nchi kavu na kwenye maji kama vile pomboo na nyangumi.

8. Mamalia wana miili yenye damu joto. Joto lao halibadiliki kulingana na mabadiliko ya halijoto ya mazingira (homeothemia).

9. Mamalia hutumia mapafu kupumua.

SURA 2: USANISHAJI CHAKULA

Maana ya Usanishaji Chakula

Usanishaji chakula ama fotosinthesisi ni kitendo cha mmea kujitengenezea chakula chake kwa kutumia hewa ya kabonidayoksaidi, maji na nishati ya mwanga wa jua. Kitendo hiki hufanyika katika sehemu maalumu ya mmea hasa zile zenye umbijani kama vile kwenye majani. Mimea yote hai ina uwezo wa kujitengenezea chakula.

Sehemu Kuu za Mmea

Mimea ina sehemu kuu tatu. Sehemu hizo ni:1. Mizizi

2. Shina

3. Majani

Sehemu Kuu za Nje za Jani na Kazi Zake

Jani lina sehemu kuu sita za nje kama ifuatazo: kikonyo, vishipajani, ncha, kingo, vena kuu na lamina.

1. Kikonyo: ni sehemu ya jani ambayo huunganisha jani na shina au tawi la mmea. Pia huunganisha vena kuu na vishipajani.

Kazi:​(i) kusafirisha maji, madini na virutubisho kutoka kwenye shina kwenda kwenye jani.

(ii) Kusafirisha chakula kilichotengenezwa na jani kwenda kwenye shina na sehemu nyingine za mmea.

2. Vishipa jani: ni vena au kishipa kidogo cha jani. Sehemu hii inayohusika zaidi katika usafirishaji kwenye jani. Kazi:​(i) kusafirisha maji, madini na virutubisho kutoka kwenye shina kwenda kwenye jani.

(ii) Kusafirisha chakula kilichotengenezwa na jani kwenda kwenye shina na sehemu nyingine za mmea.

3. Lamina: ni sehemu laini ya jani yenye seli zenye kloroplasti. Kloroplasti zina dutu za rangi ya kijani zinazoitwa klorofili, chanikiwiti au umbijani ambazo kazi yake ni kufyonza mwanga wa jua na kuubadilisha kuwa nishati ya mwanga wa jua kwa ajili ya usanishaji chakula. Lamina pia ina vishimo vidogovidogo vinavyoitwa stomata ambavyo kazi yake ni kupitisha hewa ya oksijeni, hewa ya kabonidayoksaidi na maji katika hali ya mvuke.

Kazi:​(i) Kufyonza/kusharabu nishati ya mwanga wa jua kwa ajili ya usanishaji chakula (umbijani).

(ii) Kupitisha hewa ya oksijeni, hewa ya kabonidayoksaidi na maji/mvuke kwa ajili ya usanishaji chakula.

4. Vena kuu: ni sehemu ya jani inayohusika zaidi katika usafirishaji wa malighafi za usanishaji chakula pamoja na chakula kilichotengenezwa na mmea. Sehemu hii ina vifereji vipitishi viwili viitwavyo zailemu na floemu.

Kazi:​(i) kusafirisha maji, madini na virutubisho kutoka kwenye shina kwenda kwenye jani (zailemu).

(ii) Kusafirisha chakula kilichotengenezwa na jani kwenda kwenye shina na sehemu nyingine za mmea

(floemu).

Sehemu za Ndani za Jani

Jani likikatwa mshazari na kuangaliwa kwa kutumia hadubini huonesha sehemu kama epidemisi ya juu, selisafu za kati, epidemisi ya chini.

Epidemisi ya upande wa juu na wa chini: Sehemu za ndani za jani hulindwa na utando pamoja na epidemisi za upande wa juu na chini ya jani. Utando wa chini na juu wa jani pamoja na epidemisi husaidia mwanga wa jua kupenya na kuingia kwenye sehemu za kati ya jani. Utando na epidemisi ya chini ya jani una vishimo vidogo vidogo vinavyoitwa stomata.

KUPATA NOTES KAMILI WASILIANA NASI  0675701982/0743441251/0679241251

➢ NOTES

➢ LESSON PLAN

➢ EXAMS

➢ SCHOOL ACTION PLAN

1

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *